KIKAO CHA VIUNGO VYA MWILI
Siku moja viungo vya mwili wa binadamu vilikaa kikao. Kikao hicho ilikuwa ni kuelezea masikitiko yao juu ya kiungo kimoja kilichoonekana kutokuwa na faida wala msaada kwa viungo vingine katika kutenda kazi ya kuujenga mwili. Viungo vingine vilidai kuwa kiungo hiki hakikuwa na mchango wowote zaidi ya kutumia faida ya wenzie waliokuwa wakifanya kazi sana. Kati ya viungo vilivyoshiriki alikuwepo Macho, Mdomo, Masikio, Ulimi, Miguu, Mikono na Tumbo ambaye ndiye alikuwa mlalamikiwa.
Kikao kilianza na kilikuwa na ajenda moja kuu nayo ni kumtuhumu Tumbo kwamba kwanini hasaidii wenzake na haoneshi ushirikiano kabisa, zaidi yeye hupokea tu. Macho yalianza kwa kujitapa, “Mimi ndiye bora sana kwani bila mimi huyu binadamu hawezi kuona wala kujua kitu chochote; Lakini mwenzetu Tumbo simuoni hata akishiri hata kitu chochote bora hata miguu hutembea kufuata”. Akiwa hajamilizia, Mdomo ukadakia na kusema mimi hula chakula na kutafuna na humpelekea tumbo ambaye yeye huchukua tu bila kufanya kazi. Ulimi ukasema baada ya wewe mdomo kula mimi ndiye hujua ladha ya chakula kama ni kitamu ama kichungu na huamua kiende huko kwa Tumbo ama la. Viungo vyote viliendelea kujitapata jinsi vilivyokuwa na umuhimu kwa binadamu na isipokuwa Tumbo tu.
Muda wote wa kikao, Tumbo lilikuwa kimya na halikusema chochote zaidi ya kuvisikiliza viungo vingine vilivyoonesha makeke na kujimwambafai jinsi vilivyokuwa bora katika mwili wa binadamu. Baada ya viungo vyote kujadili na kuona angalau vinasaidiana kumfanya binadamu awe kama alivyo isipokuwa Tumbo tu, basi iliamuliwa kuwa Tumbo lifukuzwe katika mwili wa binadamu maana halina faida. Tumbo lilifukuzwa na viungo vingine vikashangilia sana maana mvivu ameondolewa. Usiombe ukutane na kitu kama hiki, utaomba poo nakwambia.
Baada ya kuliondoa Tumbo viungo vingine viliendelea na majukumu yao kama kawaida. Lakini baada ya muda vikagundua kuna kitu hakipo sawa kwenye mwili wa binadamu. Mwili ulianza kukosa nguvu na viungo vingine vikawa haviwezi kufanya kazi sawa sawa. Mdomo ulishindwa wapi pa kupeleka chakula baada ya kumeza. Kitu ambacho viungo vingine vya mwili havikufahamu ni kuwa Tumbo ndilo lilikuwa likichakata chakula na kukisambaza kwenye viungo vingine vya mwili bila vyenyewe kujua. Kumbe kila kiungo kilipata virutubisho vyote vilivyokuwa vikihitajika baada ya kuchakatwa tumboni.
Hadithi inatufunza jinsi ambavyo wakati mwingine katika maisha yetu tumewaona wenzetu kuwa hawana umuhimu wowote kwetu. Yaweza kuwa katika familia, ofisini, shuleni ama katika jamii tunayoishi. Kuna wakati tumeona kuwa tuna kila kitu na hatuwahitaji aina Fulani ya watu au aina Fulani ya vitu. Tupo hapa duniani kwa kusudi lake Mwenyezi Mungu na ni kwa makusudi kabisa akatuumba watu wengi duniani, la sivyo angekuumba wewe mwenyewe tu uishi peke yako. Hivyo basi. Ule wakati ambao tunahisi kuwa Fulani hana thamani kwetu turudi na kufikiria hadithi ya Viungo vya mwili vinavyofanya kazi kwa kushirikiana na bila kutegeana wala kulaumiana.
Leo wewe unaweza kuwa Tumbo hapo ulipo. Yawezekana kabisa umuhimu wako hauonekani, lakini amini kuwa upo duniani kwa makusudi ya Mungu yeye aliyekujua kabla ya kuumbwa kwako (Yeremia 1:4–5).
Mwenyezi Mungu akushushie roho wake na akupe mapaji yake ili uishi kwa kumpendeza yeye siku zote.
Ndimi,